Saturday, September 10, 2011

PINGAMIZI JUU YA KUFUKUZWA KAZI MJUMBE KAMATI YA UTENDAJI THTU DOTTO NANDHI

PINGAMIZI LA KUFUKUZWA KAZI BWANA DOTTO NHANDI (0787103655) KINYUME NA SHERIA NA. 6 YA MWAKA 2004 YA AJIRA NA MAHUSIANO KAZINI PAMOJA NA KANUNI ZAKE

Utangulizi

Bw. Dotto Nhandi, kabla ya kufukuzwa kazi kwa barua yenye kumb. Na. UDOM/AC/PCF-177/10 ya tarehe 15 Agosti 2011, alikuwa mwajiriwa wa kudumu katika Chuo Kikuu cha Dodoma tangu tarehe 22 Septemba 2008 na kuthibitshwa baada ya kumaliza muda wa majaribio (probation) na kuthibitishwa kuanzia tarehe 18 Juni 2009. Mwajiriwa alianza kazi kwa ngazi ya ‘Tutorial Assistant’.
Kwa nyakati tofauti Bw. Dotto Nhandi amewahi kushika nyadhifa zifuatazo
i. Mwakilishi wa wafanyakazi wa Chuo cha Elimu katika Baraza la wafanyakazi tangu Aprili 2011 mpaka alipofukuzwa kazi kinyume na sheria.
ii. Mjumbe Kamati ya Utendaji ya tawi – THTU UDOM tangu Mei 2011 mpaka alipofukuzwa kazi kinyume na sheria.
iii. Mjumbe Kamati ya Utendaji katika jumuiya ya wahadhiri (UDOMASA) tangu Januari 2011 mpaka alipofukuzwa kazi kinyume na sheria.
Nafasi zote hizo ambazo ni za kuchaguliwa amekuwa akizitumikia kwa wakati mmoja na zinaonesha imani waliyo nayo wafanyakazi wenzake kwake. Mbali ya hayo ni mchapa kazi anayejituma na ni mwaminifu na kwa THTU ni mtu wa kutegemewa sana. Bw. Dotto Nhandi anamalizia shahada yake ya uzamili na amekwishakabidhi dissertation kwa ajili ya kushahishwa. Matokeo ya awali yanaonesha kuwa Bw. Dotto Nhandi amefanya vizuri sana.

Maelezo mafupi juu ya tuhuma zinazomkabili


Mnamo tarehe 14 Juni 2011 Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Chuo Kikuu cha Dodoma aliitisha kikao kupitia wakuu wa Idara kwa ajili ya ‘Teaching Practice (TP) orientation’. Kikao kiliendeshwa na Dakta T. Bali (0765740030) na Katibu alikuwa Bw. Mbegu. Baada ya kikao hicho wahadhiri walifuatilia dondoo (minutes) kupitia kwa TP coordinator kuona kama zimekwenda kwenye mamlaka husika lakini wakagundua kwamba hazikuandikwa. Ndipo baadhi ya wahadhiri wakamwomba Bw. Dotto Nhandi ayaweke mawazo ya wahadhiri kwenye maandishi ili yawasilishwe kwenye uongozi wa chuo.
Bw. Dotto Nhandi alifanya kazi hiyo tarehe 17 Juni 2011 na kuwasilisha kwa Kaimu Mkuu wa Chuo (Principal), Deans and ‘TP Coordinator’ na kuacha swala hilo lifanyiwe kazi kwa zaidi ya majuma mawili. Na kipindi hicho wahadhiri walipisha mitihani ifanyike.
Baada ya mitihani kwisha, wahadhiri wakajadiliana waitishe kikao mnamo tarehe 7 Julai 2011 saa 3 kamili asubuhi siku ambayo kimsingi ilikuwa ni mapumziko. Bw. Nhandi aliandika ujumbe wa simu kuwajulisha wahadhiri wenzake juu ya kikao.
Siku moja kabla ya kikao ambacho wahadhri walitarajia kufanya tarehe 7 Julai 2011, Bw. Nhandi alikwenda kuonana na Kaimu Mkuu wa Chuo, Dakta L. Mtahabwa ili kupata maoni yake juu ya mawazo ya wahadhiri yaliyowekwa kwenye maandishi. Mazungumzo yalichukua zaidi ya nusu saa na Kaimu Mkuu wa Chuo alishauri majibu ya bajeti yasubiriwe kutoka utawala wa Chuo Kikuu cha Dodoma (central administration). Kimsingi, Bw. Dotto Nhandi alimwelewa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu na hivyo kuondoka. Lakini kinyume na matarajio ya wengi Bw. Dotto Nhandi, siku hiyo hiyo, alipokea barua yenye kumb. Na. UDOM/COE/PCF11/2 (angalia kiambatanisho B) ikimwonya kwa tuhuma mbili: kuchochea wanataaluma kugoma (incitement) na kudharau mamlaka (insubordination) ya chuo.
Baada ya kupokea barua hiyo kwa mshangao na mshituko mkubwa, Bw. Dotto Nhandi aliwasiliana na viongozi wa UDOMASA na baadhi ya wahadhiri wa Chuo cha Elimu wakaitisha kikao ili kujiridhisha dhidi ya tuhuma alizopewa Bw. Dotto Nhandi. Kikao hicho kilijiridhisha kuwa mawazo yaliyoandikwa na Bw. Dotto Nhandi yalikuwa ni mawazo ya wahadhiri wote wa Chuo cha Elimu.
Kikao hicho kiliamua kwamba UDOMASA ifuatilie swala hilo na kuhakikisha barua hiyo ya onyo dhidi ya Bw. Dotto Nhandi inaondolewa kwenye faili kwa sababu ilitolewa kinyume na taratibu. Tarehe 13 Julai 2011 Bw. Dotto Nhandi aliandika barua ikiwa ni sehemu ya kukata rufaa na kupata fursa ya kujieleza na akapendekeza kuwa barua ya onyo iondolewe kwenye faili lake. Tarehe 14 Julai 2011 Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo alijibu kwamba onyo linabaki pale pale na kumwomba Bw. Dotto Nhandi atumie ushauri huo siku zijazo.
Tarehe 20 Julai 2011 saa 5 asubuhi, Bw. Nhandi alipokea barua yenye kumb. Na. UDOM/AC/PCF-177/9 ya tarehe 15 Julai 2011 ikimtaka afike katika Kamati ya Nidhamu ya Chuo Kikuu cha Dodoma tarehe 21 Julai 2011 kwa ajili ya kujibu tuhuma za “Breaching Public Service Regulations 42 (1) (3); 65 (1) III (i, ii, v, and vii) pamoja na “Breaching section F.26 of the 2009 Standing Orders of Public Service”.
Mnamo tarehe 18 Agosti 2011 Bw. Dotto Nhandi alipokea barua ya kufukuzwa kazi ambayo ilitokana na maazimio ya Kikao Maalum cha Baraza la Chuo la tarehe 12 Agosti 2011.

Sababu za kupinga adhabu ya kufukuzwa kazi


1. Barua ya Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu (kiambatanisho B) imekiuka sheria na. 6 ya mwaka 2004 ya ajira na mahusiano kazini; kanuni za utendaji bora za mwaka 2007 sehemu ya 6 ihusuyo mwongozo wa sera na taratibu za kushughulikia nidhamu sehemu ya 2 na 3 (T.S. Na. 42). Kimsingi Bw. Dotto Nhandi hakuwahi kupewea onyo kwa mdomo wala maelekezo yoyote kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu kama sheria inavyotaka kabla ya kupewa onyo kwa maandishi.
2. Onyo kwa maandishi kwa Bw. Dotto Nhandi lilikiuka sheria ya ajira na mahusiano kazini na kanuni zake T.S. Na. 42 mwaka 2007 ambazo zinamtaka meneja amtaarifu mwajiriwa sababu za hatua iliyochukuliwa na kumpatia mwajiriwa fursa ya kujieleza. Baada ya hapo meneja aamue kama atampatia au hatampatia mwajiriwa onyo kwa maandishi. Bw. Dotto Nhandi hakupata fursa ya kujieleza.
3. Hata Bw. Dotto Nhandi alipojaribu kutumia haki yake ya msingi kujieleza akiamini ameonewa na kushauri barua ya onyo aliyopewa iondolewe kwenye faili lake kwa sababu taratibu hazikuzingatiwa, alijibiwa kwamba onyo lipo pale pale. Pamoja na kumkumbusha Bw. Dotto Nhandi, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu aliendelea kuvunja sheria na kanuni zake (kanuni za utendaji bora) T. S. Na. 42 ya tarehe 16 Februari 2007.
Pia Bw. Dotto Nhandi, kupitia barua yake ya kujitetea dhidi ya onyo alilopewa, aliomba apatiwe barua ya kumtaka radhi kwa tuhuma nzito za uchochezi wa mgomo na kudharau mamlaka akiamini fika kwamba yaliyofanywa yalikuwa ni kwa ajili ya kujenga; na ikizingatiwa kwamba hakuna mahali hapo chuoni amani ilivunjika au uharibifu wowote kutokea. Hapa alikuwa akitumia haki yake ya msingi ya kujieleza na kujitetea kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, alijibiwa kuwa onyo lipo pale pale kupitia barua ya tarehe 14 Julai 2011.
4. Bw. Dotto Nhandi aliitwa kwenye kikao cha Kamati ya Nidhamu ya Chuo Kikuu cha Dodoma tarehe 21 Julai 2011 kupitia barua aliyopewa tarehe 20 Julai 2011 saa 5 kamili asubuhi. Hapa alinyimwa haki ya msingi (natural justice) ya kuweza kupata muda wa kutosha kwa ajili ya kuandaa utetezi wake. Sheria inataka angalau masaa 48. Kutokana na kunyimwa muda pia Bw. Dotto Nhandi alishindwa kwenda na shahidi wake kama sheria inavyotoa fursa hiyo.
5. Swala la Bw. Nhandi lilikwenda moja kwa moja kwenye Kamati ya Nidhamu pamoja na kwamba uongozi wa Chuo cha Elimu haukushauri swala hilo lifikishwe kwenye kamati hiyo. Barua iliyoandikwa tarehe 14 Julai 2011 na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu ikiwa ni majibu kwa Bw. Dotto Nhandi ilisisitiza kuwa onyo lilibaki pale pale na hakuna maelezo yoyote kwamba swala hili lingepelekwa katika Kamati ya Nidhamu. Swala la Bw. Nhandi halijajadiliwa na vikao husika vya Skuli au Chuo cha Elimu na hata hayajafika kwenye Kamati ya Rasilimali Watu kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine.
Ikiwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu aliridhika, kupitia barua yake yenye kumb. Na. UDOM/COE/PCF 11/2 ya tarehe 6 Julai 2011 kwenda kwa Bw. Dotto Nhandi; na hakuna kikao chochote ngazi ya Chuo cha Elimu kilichoomba swala la Bw. Dotto Nhandi lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu, je nani aliyependekeza hatua hiyo? Hatutaki kuamini kuwa swala hili limeibuliwa kwa hila.
6. Kikao maalum cha Baraza la Chuo kilichofanyika tarehe 12 Agosti 2011, ambacho ndicho kiliridhia kufukuzwa kwa Bw. Dotto Nhandi, kilifanyika baada ya taarifa iliyotolewa muda mfupi sana kabla ya kikao chenyewe. Mwakilishi wa jumuiya ya wahadhiri, Bw. Paul Loisulie (0755210310) alipewa taarifa saa 3 asubuhi na kikao kikafanyika saa 4 asubuhi ya siku iyo hiyo. Hali hiyo pia ilinyima fursa ya kuandaa utetezi (natural justice) kwa ajili ya watu anaowawakilisha, Bw. Dotto Nhandi akiwa mmoja wao. Tunashawishika kuamini kwamba kikao hiki kimefanyika kwa hila na hivyo kuzuia natural justice.
7. a). Tarehe 18 Agosti 2011 Bw. Dotto Nhandi alipokea barua ya kufukuzwa kazi yenye kumb. Na. UDOM/AC/PCF-177/10 ya tarehe 15 Agosti 2011 akihukumiwa kwa kutotii mamlaka na hivyo kukiuka ‘First Schedule of the Public Service Regulation 42 (3) na kanuni za kudumu za utumishi wa umma na. F.27 (1) C. Kosa ambalo kimsingi Bw. Dotto Nhandi halikubali. Barua hiyo haionyeshi kuwa Bw. Dotto Nhandi alifukuzwa kwa kutumia vifungu gani vya adhabu au kwa kutumia sheria ipi.
b). Kwenye barua hiyo anaombwa alipe mkopo ambao dhamana yake ilikuwa ni ajira kwa maana ya mshahara na chuo kilidhamini kwa asilimia 100 iwapo angeshindwa kulipa. Bw. Dotto Nhandi hawajibiki kwa namna yoyote ile kulipa deni hilo kwa kuzingatia mkataba uliokuwepo kati ya chuo na benki husika (CRDB).
8. Kamati ya Utendaji ya THTU – UDOM imepitia vielelezo vyote ikiwemo barua ya kufukuzwa kazi na kuangalia taratibu zote zilizotumika kwa ufupi zinapingana na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 22 na sheria na. 6 ya mwaka 2004 ya ajira na mahusiano kazini na kanuni zake.

Ushauri na mapendekezo

1. Uongozi wa THTU tawi la UDOM na uongozi wa UDOMASA unafanya jitihada za kukutana na mwenyekiti wa Baraza la Chuo kuona kama kuna uwezekano wa kutengua adhabu hii. Hii ni njia mojawapo ya kidiplomasia ingawa haipo kwa mujibu wa sheria.
2. Wakati tukiendelea na shauri la awali, tunaiomba THTU makao makuu, kupitia mwanasheria wake Dakta Sengondo Mvungi, itusaidie kulifikisha swala hili kwenye Baraza la Usuluhishi kwa mujibu wa sheria ya kazi Na. 6 ya 2004 sehemu ya 86.
3. Ikiwa hatutafanikiwa na mazungumzo na mwenyekiti wa Baraza la Chuo, tutamsaidia Bw. Dotto Nhandi kukata rufaa kwenye kamati ya rufaa ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
4. Ikiwa hakuna mafanikio hata katika Baraza la Usuluhishi, tunaomba na tumejiandaa swala hili lipelekwe katika mahakama ya kazi kama inavyoelezwa na sheria ya ajira na mahusiano kazini sehemu ya 94.
5. Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa haki itatendeka kwenye moja ya mapendekezo hapo juu. Hata hivyo, tupo tayari swala hili lipelekwe hata mahakama ya rufaa ikiwa hatua zote za chini zitashindikana.
Tunataka haki itendeke na ionekane kuwa imetendeka.

NIA NA MWELEKEO WETU DAIMA NI KUJENGA

Nawasilisha,

Iddy Mwerangi
Mwenyekiti – THTU UDOM

2 comments:

  1. Suala la Dotto, tayari limekamilika na Juzi, 24 Septemba 2011, tulikutana nae kwa mwanasheria, tukafanya viapo vyote, na tukaandikishiana SPECIAL POWER OF ATTORNEY, na tayari tumeikabidhi hati kwa msajili.

    Kuanzia sasa tuna mamlaka yote kisheria kufuatilia, kuhoji, kusimamia, kushitaki, kupinga na kumuwakilisha katika masuala mengine yote ya DOTTO, yanayohusu kufukuzwa kwake kazi.

    Kazi hiyo tayari tumeianza na sasa kesi ipo CMA (Court of Mediation & Arbitration. Tunaomba tuendelee kushirikiana katika hili, naamini tutashinda.

    ReplyDelete
  2. Kesi ya Mwanaharakati Dotto Nandhi, itaanza kusikilizwa CMA, siku ya Jumatano, tarehe 2 Novemba 2011. Naomba tuendelee kushirikiana.

    Kwa sasa Mjumbe kamati ya Utendaji THTU, Bwn, LOISULIE, Paul anamalizia kuandaa taratibu za ufunguzi wa kesi ya Calist Ritte, Jumatatu itakabidhiwa CMA, kwa ajili ya rufaa.

    ReplyDelete

Note: Only a member of this blog may post a comment.