Friday, October 28, 2011

RUFAA YA CALIST RITTE JUU YA KUACHISHWA KAZI ISIVYO HALALI

A: UTANGULIZI

Calist Ritte aliajiriwa Chuo Kikuu cha Dodoma mnamo tarehe 05 Septemba 2007 kupitia barua yenye kumbukumbu Na. DVC/AC/AP/07/13 kama Tutorial Assistant.Kabla ya kuajiriwa UDOM,Calist Ritte alikuwa muajiriwa wa wizara ya elimu akifundisha shule ya sekondari ya wasichana Ashira.

Mnamo 25th October 2007,Calist alimwandikia barua katibu mkuu kumjulisha juu ya ajira yake mpya na kumuomba asimamishe mshahara ,na nakala ya barua hiyo ilitumwa kwa katibu mkuu wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi.Akiwa wizara ya elimu file lake ni namba EDPF 29957 na check 9343030.

Pamoja na kuandika barua mshahara uliendelea kuanzia Septemba 2007 hadi Machi 2008 ambapo ulisimamishwa. Hatua hiyo ilimridhisha kwamba ombi lake lilishaanza kushughulikiwa. Cha kustaajabisha Machi 2009 mshahara ulirudishwa tena bila kupewa taarifa yoyote, hadi July 2010, alipogundua mshahara kutoka MoEVT umeanza kurudi tena aliaandika barua tarehe 22/04/2010 kuusimamisha, hakujibiwa hadi Agosti 2010 kupitia barua yenye Kumb. Na. CB. 45/169/01/ ‘S’/27 kutoka Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma ikimtaka arudishe mishahara na nakala ilitumwa kwa Mkuu wa Chuo, Chuo Kikuu Dodoma.

B: TUHUMA ZINAZOMKABILI

Calist Ritte anatuhumiwa kuvunja kanuni za maadili za chuo Na. 6, kwa udanganyifu, na pia ametuhumiwa kwa udanganyifu mkubwa (Gross dishonesty) F. 27 (kanuni za kudum u za utumishi wa umma). Udanganyifu unahusu kupokea mishahara miwili, moja kutoka kwa mwajiri wake wa zamani, (MoEVT) na pili mwajiri wa sasa UDOM kati ya Septemba 2007 hadi Februari 2008 na Machi 2009 hadi Julai 2010.

Tuhuma tajwa hapo juu zinapatikana kwenye barua kutoka Utumishi yenye namba CB. 45/169/01/ ‘S’/27 ya 03 Agosti 2010, na barua kutoka UDOM yenye Kumb. Na. UDOM/AC/PCF-103/12 ya tarehe 15 Agosti 2011. Alipokea barua ya kufukuzwa kazi tarehe 22 Septemba 2011 yenye Kumb. Na. UDOM/AC PCF 147/14 ya tarehe 06 Septemba 2011.

C: SABABU ZA KUPINGA KUFUKUZWA KAZI

Tuhuma zinazomkabili si sahihi, ikumbukwe mwajiriwa hawezi kujitoa mwenyewe kwenye orodha ya malipo; ikichukuliwa Calist Ritte amefanya jitihada za kutosha kumtaarifu mwajiri wake wa zamani.

1. Tarehe 25 Oktoba 2007, aliandika barua Utumishi na nakala kwenda Wizara ya Elimu, barua ambayo hakujibiwa, pamoja na kufanya ufuatiliaji mara kadhaa Wizarani mshahara ulisimamishwa mwezi Machi 2008, na Ritte alijua suala hili limekwisha. Mwezi Machi 2009 mshahara ulianza kuingizwa tena kwenye akaunti ya Calist Ritte bila yeye kujua.

2. Tarehe 22 Aprili 2010 aliandika tena barua Utumishi akikumbushia barua yake ya awali ya tarehe 25 Oktoba 2007, na akiomba mshahara wake usitishwe. Barua hii ilijibiwa miezi minne baadaye kupitia barua yenye Kumb. Na. CB.45/169/01/ ‘S’/27 ya tarehe 03 Agosti 2010 ikimtaka kurudisha mishahara husika.
Hili halina shaka limefanyika kwa ajili ya uzembe wa mwajiri kushindwa kushughulikia barua kwa wakati.

3. Barua zote ambazo Ritte ameandikiwa zikimtaka arudishe kiwango hicho, hazitaji ni kiasi gani anachodaiwa, hivyo itakuwa ni vigumu kuanza kulipa.

4. Calisti Ritte aliitwa kwenye kamati ya nidhamu kwa kupigiwa simu na hakuambiwa makosa yake, na alipigiwa siku hiyohiyo. Hapa alinyimwa haki ya msingi ya kuweza kupata muda wa kutosha kwa ajili ya utetezi. Uongozi wa Chuo ulivunja kanuni za ajira na mahusiano kazini (13) (3).

5. Mwanzoni mwa mwaka 2011, Ritte aliomba mkopo benki ya CRDB, kupitia dhamana ya Chuo, alinyimwa kwa madai ana tuhuma za kupokea mishahara miwili. Uongozi wa Chuo badala ya kumfukuza kazi ungemruhusu akope ili alipe hiyo hela.

6. Kufukuzwa kazi hakukuwa sahihi, Calist Ritte angeweza kukatwa kidogokidogo kwenye mshahara wake kila mwezi ili kufidia fedha hiyo.

7. Calist Ritte amefukuzwa kazi kwa kudaiwa fedha ambayo takribani milioni nne tu, deni amabalo sio kusudio lake. Chuo kinamfukuza na kuamua kumlipa mafao ambayo ni zaidi ya milioni sita. Hapakuwa na sababu ya kufukuzwa kazi. Aidha, Chuo kingemlipia deni halafu utaratibu wa kukatwa kwenye mshahara ungeendelea. Hii inamaanisha Chuo kimeingia hasara, nabado kitaingia hasara kuajiri mfanyakazi mwingine.

8. Kamati ya nidhamu na baadae baraza la Chuo, havikutenda haki; huwezi kumwambia mwajiriwa alipe deni kubwa hivyo ndani ya siku saba tu. Mshahara wa zaidi ya miezi 20. Pamoja na hilo Calist Ritte alijitahidi na alionyesha nia akalipa shilingi 800,000/= (shilingi laki nane tu), kiwango hicho ni kikubwa sana ni zaidi ya fedha taslimu anayopokea kila mwezi na aliandika barua kueleza hilo.

9. Hakukuwa na sababu ya msingi Calist Ritte kupelekwa kwenye kamati ya nidhamu kwasababu alipoandikiwa barua na chuo yenye Kumb. Na. UDOM/AC/DCF 103/8 ya Jumapili 20 Machi 2011, ambayo aliipokea tarehe 24 Machi 2011, aliijibu vizuri sana kwenye barua yake ya tarehe 29 Machi 2011 kwa kutoa maelezo ya kina.

10. Calist Ritte hakuelezwa juu ya adhabu ya kufukuzwa na hakupewa nafasi ya kujitetea kwa nini asifukuzwe kazi, kama inavyoelekezwa na kanuni za Ajira kazini .

11. Pamoja na kwamba tuhuma zilizomtia hatihani si sahihi, kiutaratibu na hata kimazingira ya kosa lenyewe, Calist Ritte alihitaji kufikiriwa zaidi na suala lake busara kubwa itumike kwa kuwa:
i. Hivi karibuni tarehe 29 Agosti 2011 alifiwa na mama yake mzazi, akiwa anaishi nae na amemuuguza muda mrefu. Kwa hiyo hali yake ya uchumi imeyumba sana.
ii. Ni mwaka wanne sasa anahangaika kujisomesha mwenyewe Shahada ya Uzamili inayofanya kipato chake kupungua.
iii. Ana mkopo ambao alikuwa anaendelea kuulipa katika benki ya CRDB.
iv. Ana mke na watoto watatu (3).

MAONI NA MAPENDEKEZO

1. Adhabu hiyo itenguliwe, Calist Ritte arudishwe kazini.
2. Wizara ieleze wazi ni kiasi gani Calist Ritte anadaiwa; kisha taratibu za ulipaji madeni kwa wafanyakazi wa umma zifuatwe.
Nawasilisha.

“NIA NA MWELEKEO WETU DAIMA NI KUJENGA”
………………………………………………
PAUL LOISULIE
(Mjumbe Kamati ya Utendaji – (THTU)

Tuesday, October 4, 2011

Over (86) Career Opportunities Available at MAKERERE UNIVERSITY

Career Opportunities at Makerere University

KIKAO CHA THTU NA MHE. WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII KILICHOFANYIKA TAREHE 29/09/2011 DSM

Mshikamano Wajumbe,

Baada ya viongozi wa THTU kutoa tamko lao kuhusu mgogoro wa ISW kwenye vyombo vya habari ndipo Waziri wa Afya alivyowaita viongozi wa THTU na kufanya nao kikao tarehe 29/09/2011 na ifuatayo ni attachment ya THTU kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.


KIKAO CHA THTU NA MHE. WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII
KILICHOFANYIKA TAREHE 29/09/2011 DSM.


Chama cha THTU kimejihusisha na mgogoro wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii
kikamilifu na kimefanya utafiti wa kina na kubaini kwamba matatizo ya Taasisi
ya Ustawi wa Jamii yanaweza kumalizika na Taasisi kupatiwa ithibati na kurejea
katika hali ya kawaida iwapo yafuatayo yatafanyika kwa haraka:-

(i) Kuwarudisha wafanyakazi wote 30 waliofukuzwa kazi bila masharti
yoyote.

(ii) Kuwaondoa Viongozi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii ambao hawana sifa
kwa mujibu wa NACTE na ambao ndiyo chanzo cha matatizo, na
kuweka viongozi wenye sifa ili Taasisi irejee katika hali yake ya kawaida.

(iii) Kurekebisha Bodi ya Magavana ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa kuwa
haikidhi matakwa ya Bodi ya Taasisi ya Elimu ya Juu ikiwa ni pamoja na
kutokuwa na wawakilishi wa Wanataaluma, chama cha Wafanyakazi na
Baraza la Wafanyakazi.

(iv) Mhe. Waziri atengue maamuzi yaliyofanywa yakubadilisha mwakilishi wa
NACTE katika Bodi ya Magavana.

(v) Mhe. Waziri atuhakikishie kwamba Wizara na Bodi ya Magavana
wataheshimu maagizo ya NACTE na kuhakikisha kwamba yanatekelezwa.

(vi) Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itambue kwamba Taasisi ya Ustawi wa
Jamii ni Taasisi ya Elimu ya Juu na si Idara mojawapo ya Wizara na Wizara
iisimamie Taasisi kwa kupitia Bodi ya Magavana.

(vii)Mhe. Waziri atuhakikishie kwamba Wizara, Bodi ya Magavana na
Menejimenti hawaingilii shughuli za vyama vya wafanyakazi.

NIA NA MWELEKEO WETU DAIMA NI KUJENGA!
“TAIFA KWANZA”